Asubuhi tuamkapo
Mchana tuzungukapo
Na usiku tulalapo
Twajiuliza ni vipi?
Jana ilienda wapi?
Kesho mejificha wapi?
Leo tunaishi vipi?
Twajiuliza ni vipi?
Kuzaliwa salmini
Kuishi kwa Imani
Kifo na huzuni
Twajiuliza ni vipi?
Duniani mabilioni
Hewa safi mapafuni
Yatutosha sote aushini
Twajiuliza ni vipi?
Maisha kama maua
Furaha ndo kuchanua
Kunyauka ndo kuua
Twajiuliza ni vipi?
Wazee na wachanga
Wote wenda kwa mchanga
Rutuba kwa mimea kuchanga
Twajiuliza ni vipi?
Nini sababu ya maisha
Tambua kabla kuisha
Shugli zote kusitisha
Twajiuliza ni vipi?
Kifo ni nini hasa?
Kuhuzunisha kukwasa
Eti dhawabu ya anasa
Twajiuliza ni vipi?
Tajiri wabobea
Masikini kulemea
Wote kaburi lategea
Twajiuliza ni vipi?
Wema wafa mapema
Wabaya waishi vyema
Roho zote zalazwa pema
Twajiuliza ni vipi?
Ulimi mdogo kama ufa
Ila yaweza bomoa taifa
Yatoa laana na sifa
Twajiuliza ni vipi?
Wadhambi wakuu duniani
Mkombozi katoka mbinguni
Kwa niaba yetu kufa msalabani
Twajiuliza ni vipi?
Tulianguka dhambini
Wokovu hatukudhamini
Ila tuliupata kwa damu mtini
Twajiuliza ni vipi?
Hatufahamu ya mbinguni
Ila twaishi kwa tumaini
Twaogopa ya kuzimuni
Twajiuliza ni vipi?
Mema ni ya mbinguni
Mabaya ya kuzimuni
Yote metenda bado ya hukumuni
Twajiuliza ni vipi?
Kila siku twajiandaa
Mbinguni sote kupaa
Ila twajua hatujafaa
Twajiuliza ni vipi?
Tambua leo basi
Kuwa bado kuna nafasi
Wa mbingu na kuzimu farasi
Zangoja utende mema ama uasi
Mungu yupo kikweli
Ibilisi pia yupo ukifeli
Ndiye mkuu wa utapeli
Mwabudu mungu anastahili