TUMECHOKA
By Yegon Emmanuel
Nyoyo zetu zatokota, kwa uchungu tunalia
Hisia zetu zazorota, kwa maombolezo mtawalia
Kila kukicha twashituka, kwa habari za tanzia
Kwa majonzi tumechoka, wakenya twaangamia
Nchi yetu ya Kenya, tukufu na ya kifahari
Tumejivunia kuwa wakenya, tumelienzi taifa letu kwa ari
Sasa twavumilia kuwa wakenya, kwa kukosa imani na shari
Ukosefu wa usalama Kenya, umesababisha vifo vya wanahari
Majanga na mauaji, yamepata makao nchini
Ugaidi na ubakaji, umekita kambi mashinani
Tokea Garissa kaskazini, hadi mpeketoni kusini
Vijijini na mijini, kote kote hakuna amani
Ni wapi tutaenda, tumkimbilie nani?
Wa polisi kamanda, wakenya tufanyeni?
Rais wa jamhuri, hadi lini jamani?
Wachanga wenda kwenye kaburi, wauawa kihayawani.
Ajali mabarabarani, zatumaliza kukicha
Ufisadi maafisini, zatukosesha kazi
Ukabila mashinani, ni vita kila mara
Ugaidi umeingia vyuoni, wanafunzi wauawa ovyo
Tutalia hadi lini, swali langu nauliza
Wanafunzi masomoni, bila makosa kuangamiza
La kusikitisha serikalini,ni idadi kugeuza
Na kupuuza ilani, kwa maafisa wa usalama
Hadi tama nimefika, kwa sala kuhitimisha
Roho zao akina kaka, maulana azilaze pema
Familia zao kwa hakika, mterehemezi awape rehema
Na ya Kenya serikali, tambueni wakenya TUMECHOKA!