
Asubuhi na mapema
Tuliamka kwa wema
Tukamshukuru mungu mwema
Kwa maisha na rehema
Vitambulisho na kura mikononi
Tukaelekea vituoni
Siku nzima kwenye foleni
Tukapiga kura kwa amani
Matokeo yalitutuia mashakani
Tukafurushwa toka manyumbani
Nyumba zikateketea motoni
Katulazimu kwenda ukimbizini
Tulikosa Amani nchini
Vita, mauaji nyumbani
Wasiwasi kilio maishani
Uganda katupa maskani
Miaka nane ukimbizini
Maisha magumu kambini
Kisha tukapelekwa kaskazini
Tukapewa mashamba yakini
Watoto wakaenda shuleni
Wakasoma kufika shuleni
Ukulima tukafanya shambani
Vyakula tukapata ghalani
Serikali zikaja patana
Turejee nyumbani kakubaliana
Furaha tulipata kwa asana
Tumaini la ndugu kuonana
Ahadi tulipewa za kutosha
Vyeti vya shule kubadilisha
Vitambulisho kwa vijana kuhakikisha
Mashamba yetu kurejesha
Mambo yakageukia malaba
Tulipata vitisho si haba
Kinyume na ule mkataba
Tulifurushwa shida zetu kubeba
Tuliagizwa turudi makwetu
Kapewa nauli twende zetu
Yakapuuzwa mahitaji yetu
Tukaomba makao kwa wenzetu
Baada ya miezi mingi kuteseka
Kuombaomba kweli tukachoka
Pamoja na viongozi tukatoka
Kuelekea jiji kuu tukafika
Juhudi za kumuona rais zilifeli
Tukahisi kuwa katutapeli
Kupuuzwa kulituuma kweli
Matumaini yakafika mwisho wa reli
Wakati wote hatuna mahala
Pa kula wala pa kulala
Hatimaye nje ya bunge tukatawala
Kwa baridi tukikesha kwa sala
Mchana jua kali lituchoma
Usiku mvua na baridi litusakama
Wapita njia kwa dharau litutazama
Vyakula tulipewa na wasamaria wema
Wanahabari walitutembelea
Kutuhoji, habari tukawaelezea
Ila bado wengi walitukemea
Kutuita Waganda wanaonyemelea
Chakula na maji kupata taabu
Ilikua vigumu kupata matibabu
Usiku mmoja mtoto kazaliwa kwa taabu
Hospitalini mama kafukuwa bila sababu
Usiku tulikosa amani
Kwa kuvamiwa gizani
Kuagizwa kuondoka bungeni
Vitisho kila siku maishani
Baada ya mwezi mzima
Kukaa kwetu kukafika hatama
Tulifurushwa usiku wa manane
Kwa ukatili tukalazimishwa kuhama
Machifu na polisi walitufukuza
Kama mizigo kwa lori kutubwaga
Wengine wetu wakaumizwa
Kwa kupigwa bila huruma
Tukaachwa kichakani Nakuru
Wenzetu wakisalia jijini
Stakabadhi zetu walitupora
Tumesalia wakimbizi nchini
Wenzetu walokua jijini
Wameungana nasi Nakuru
Kwa usaidizi wa wasamaria wema
Makanisa metupa makao ya muda
Ila kwa yote hatuna kosa
Kuagiza haki zetu kumetuletea mikasa
Kosa tulilofanya ni kupiga kura
Machafuko yalofuatia yakatugeuza wakimbizi
Yauma kuwa mkimbizi katika nchi yako
Ulikozaliwa, ukalelewa na kuishi
Kisha kukataliwa na serikali uliyoichagua
Uchaguzi ambao ulikugeuza mkimbizi
Twatoa wito kwa serikali
Rais Kenyatta na naibu wake Ruto
Kumbukeni miadi mliyofanya
Tambueni tena sisi ni wakenya
Hatufahamu yajayo kesho
Maisha kweli kama moshi
Wasiwasi, njaa magonjwa na woga
Ila kwa yote twamshukuru maulana
Thamani ya uzalendo